Jeremiah 50:15-29

15 aPiga kelele dhidi yake kila upande!
Anajisalimisha, minara yake inaanguka,
kuta zake zimebomoka.
Kwa kuwa hiki ni kisasi cha Bwana,
mlipizeni kisasi;
mtendeeni kama alivyowatendea wengine.
16 bKatilieni mbali mpanzi kutoka Babeli,
pamoja na mvunaji na mundu wake akivuna.
Kwa sababu ya upanga wa mdhalimu
kila mmoja na arejee kwa watu wake mwenyewe,
kila mmoja na akimbilie
kwenye nchi yake mwenyewe.

17 c“Israeli ni kundi lililotawanyika
ambalo simba wamelifukuzia mbali.
Wa kwanza kumla alikuwa mfalme wa Ashuru,
wa mwisho kuponda mifupa yake
alikuwa Nebukadneza mfalme wa Babeli.”
18 dKwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo:

“Nitamwadhibu mfalme wa Babeli na nchi yake
kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.
19 eLakini nitamrudisha Israeli katika malisho yake mwenyewe
naye atalisha huko Karmeli na Bashani;
njaa yake itashibishwa
juu ya vilima vya Efraimu na Gileadi.
20 fKatika siku hizo, wakati huo,”
asema Bwana,
“uchunguzi utafanyika kwa ajili ya kosa la Israeli,
lakini halitakuwepo,
kwa ajili ya dhambi za Yuda,
lakini haitapatikana hata moja,
kwa kuwa nitawasamehe
mabaki nitakaowaacha.

21 g“Shambulieni nchi ya Merathaimu
na wale waishio huko Pekodi.
Wafuatieni, waueni
na kuwaangamiza kabisa,”
asema Bwana.
“Fanyeni kila kitu nilichowaamuru.
22 hKelele ya vita iko ndani ya nchi,
kelele ya maangamizi makuu!
23 iTazama jinsi nyundo ya dunia yote
ilivyovunjika na kuharibika!
Tazama jinsi Babeli ilivyokuwa ukiwa
miongoni mwa mataifa!
24 jNimetega mtego kwa ajili yako, ee Babeli,
nawe ukakamatwa kabla haujafahamu;
ulipatikana na ukakamatwa
kwa sababu ulimpinga Bwana.
25 k Bwana amefungua ghala lake la silaha
na kuzitoa silaha za ghadhabu yake,
kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mwenye Nguvu Zote
anayo kazi ya kufanya
katika nchi ya Wakaldayo.
26 lNjooni dhidi yake kutoka mbali.
Zifungueni ghala zake za nafaka;
mlundikeni kama lundo la nafaka.
Mwangamizeni kabisa
na msimwachie mabaki yoyote.
27 mWaueni mafahali wake wachanga wote;
waacheni washuke machinjoni!
Ole wao! Kwa kuwa siku yao imewadia,
wakati wao wa kuadhibiwa.
28 nWasikilizeni watoro na wakimbizi kutoka Babeli
wakitangaza katika Sayuni
jinsi Bwana, Mungu wetu alivyolipiza kisasi,
kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.

29 o“Waiteni wapiga mishale dhidi ya Babeli,
wote wale wavutao upinde.
Pigeni kambi kumzunguka kabisa,
asitoroke mtu yeyote.
Mlipizeni kwa matendo yake;
mtendeeni kama alivyotenda.
Kwa kuwa alimdharau Bwana,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.
Copyright information for SwhNEN